Watu 12 wauawa na kujeruhiwa katika maandamano ya 'kujitenga' Cameroon
Kwa akali watu sita wameuawa na wengine sita wamejeruhiwa na askari wa jeshi la Cameroon, wakati wa maandamano ya kushinikiza kujitenga maeneo ambayo wakazi wake wanazungumza Kiingereza, katikati mwa nchi.
Meya wa mji wa Kumbo, Donatus Njong Fonyuy ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, miongoni mwa wanaharakati waliouawa katika maandamano hayo ya jana Jumapili ni wafungwa watano waliokuwa wakijaribu kutoroka jela.
Amesema jeshi la nchi hiyo aidha limeua kwa kumfyatulia risasi mtu mmoja aliyekuwa akiandamana, alipojaribu kunyanyua bendera ya harakati ya Ambazonia inayoshinikiza kujitenga majimbo hayo ambayo raia wake wanazungumza Kiingereza.
Raia wachache wa Cameroon wanaozungumza lugha ya Kiingereza wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara tangu Novemba mwaka jana wakilalamikia kutengwa na serikali ya nchi hiyo.
Wafanyakazi wengi wa umma katika maeneo hayo pia wamekuwa wakifanya mgomo kulalamikia kile wanachokitaja kama ubaguzi, ambapo wanasema raia wa Cameroon wanaozungumza Kifaransa ndio wamekuwa wakipewa nafasi za ajira.