Maelfu ya raia wa Congo wakimbilia Zambia kutokana na machafuko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35199-maelfu_ya_raia_wa_congo_wakimbilia_zambia_kutokana_na_machafuko
Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbilia nchi jirani ya Zambia katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita wakikimbia ghasia na machafuko yanayoendelea nchini kwao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 04, 2017 02:23 UTC
  • Maelfu ya raia wa Congo wakimbilia Zambia kutokana na machafuko

Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbilia nchi jirani ya Zambia katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita wakikimbia ghasia na machafuko yanayoendelea nchini kwao.

Hayo yametangazwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ambalo limesisitiza kuwa, zaidi ya raia 3,360 wa Congo wamelazimika kukimbilia Zambia tangu tarehe 30 mwezi wa Agosti kutokana na machafuko, kiwango ambacho shirika hilo kinasema ni kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Msemaji wa UNHCR, Andrej Mahecic amesema raia hao wanakimbia mapigano ya kikabila, pamoja na mapigano kati ya vikosi vya usalama vya Congo na makundi ya wanamgambo.

Mahecic ameongeza kuwa, raia wa Congo wanaowasili Zambia wanasema kuwa wamekabiliana na ukatili uliopindukia, na kwamba raia wanauawa, wanawake wanabakwa, mali za raia zinaporwa na nyumba zao zinachomwa moto.  

Ripoti zinasema idadi kubwa ya wakimbizi hao ni kutoka kaskazini mwa mikoa ya Tatanga na Tanganyika.

Katika miaka ya hivi karibuni maeneo hayo yamekuwa uwanja wa mapigano ya umwagaji damu kati ya mbilikimo na watu wa kabila la Luba.