Wanamgambo 10 wauawa katika mapigano na jeshi la Kongo DR
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuuawa wanamgambo 10 katika mapigano na jeshi la nchi hiyo.
Kwa mujibu wa habari hiyo, mapigano kati ya jeshi la Kongo DR na wanamgambo wa Mai Mai yamejiri katika eneo la Lubero karibu na mji wa Goma, katika mkoa wa Kivu Kaskazini ambapo kuna makundi mengi ya wanamgambo waasi wa ndani na nje ya nchi hiyo. Jules Tshikudi, msemaji wa jeshi la Kongo katika mkoa wa Kivu Kaskazini amewataka wanamgambo hao kuweka chini silaha zao na kufuata mkondo wa amani.
Kadhalika Tshikudi ameelezea kuuawa askari mmoja wa serikali katika mapigano hayo na kwamba jeshi hilo bado linaendelea na operesheni ya kulisafisha eneo hilo la Lubero kutokana na uwepo wa wanamgambo wanaobeba silaha. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, waasi wa serikali wamekuwa wakishambulia mara kwa mara kambi za jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hivyo kusababisha mauaji ya askari kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa. Hayo yanajiri katika hali ambayo maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbilia nchi jirani ya Zambia katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kutokana na ghasia na machafuko yanayoendelea nchini mwao.