Tunisia yasambaratisha genge jingine la kigaidi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imetangaza kuwa, imesambaratisha genge moja la ukufurishaji lenye mfungamano na kundi la kigaidi linalojulikana kwa jina la Answar al Sharia.
Shirika la habari la ISNA limenukuu taarifa iliyotolewa na wizara hiyo ikisema kuwa, vikosi vya ulinzi wa taifa vya Tunisia vimefanikiwa kuwatia nguvu wanachama sita wa genge moja la wakufurishaji na katika usaili watu hao wamekiri kuwa ni wanachama wa genge la kigaidi la Answar al Sharia.
Wizara hiyo imeongeza kuwa, magaidi hao wametiwa mbaroni katika eneo la bin Arus, kaskazini mwa Tunisia. Kundi hilo limekuwa likiwawachochea vijana kujiunga na magenge ya kigaidi na kufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, baada ya mwendesha mashtaka mkuu kuingia kwenye kesi hiyo, inabidi hatua zote za kisheria kuhusiana na magaidi hao zichukuliwe. Hivyo uchunguzi bado unaendelea.
Raia wengi wa Tunisia ni wanachama wa magenge ya kigaidi katika maeneo tofauti duniani. Hivi sasa serikali ya Tunis ina woga wa kurejea nchini humo karibu raia wake elfu tano waliojiunga na magenge ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS) nje ya Tunisia.