Wapinzani Guinea Bissau waandamana wakitaka serikali ya Rais Vaz ijiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35999-wapinzani_guinea_bissau_waandamana_wakitaka_serikali_ya_rais_vaz_ijiuzulu
Mamia ya wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Guinea Bissau wamefanya maandamano katika mji mkuu Bissau kushinikiza kujiuzulu serikali ya Rais Jose Mario Vaz wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 28, 2017 04:32 UTC
  • Wapinzani Guinea Bissau waandamana wakitaka serikali ya Rais Vaz ijiuzulu

Mamia ya wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Guinea Bissau wamefanya maandamano katika mji mkuu Bissau kushinikiza kujiuzulu serikali ya Rais Jose Mario Vaz wa nchi hiyo.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, waandamanaji hao zaidi ya elfu moja kutoka vyama 18 vya upinzani walifanya maandamano hayo jana Ijumaa, wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kumkashifu rais wao.

Hata hivyo uwepo wa maafisa wa usalama katika kila pembe ya mji huo ulifanya maandamano hayo yasinoge, na yakaonekana tu kama mkusanyiko mkubwa wa watu.

Mmoja wa waandamanaji hao kwa jina Pereira amenukuliwa na waandishi wa habari akisema: "Hiki ni kionjo tu, maandamano makubwa zaidi yataendelea kushuhudiwa katika jiji hili hadi Novemba 5. Tunatumai kuwa jeshi, asasi za kirai na makundi ya kidini yataungana na sisi katika maandamano haya."

Rais Jose Mario Vaz wa Guinea Bissau

Mwezi uliopita wa Septemba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa sanjari na kuelezea wasiwasi mkubwa lilionao kuhusiana na mkwamo wa kisiasa wa Guinea Bissau, liliwataka viongozi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika watafute haraka iwezekanavyo njia ya ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Mgogoro wa kisiasa nchini Guinea Bissau uliibuka Agosti mwaka 2015 baada ya Rais  José Mário Vaz kumuuzulu Waziri Mkuu Domingos Simoes Pereira na kumchagua mtu mwingine kushika wadhifa huo. Rais  Vaz alimuuzulu Pereira akimtuhumu kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma;  tuhuma ambazo zilikanushwa vikali na makundi ya kisiasa ambayo ni wafuasi wa mwanasiasa huyo.