Wakenya wanasubiri matokeo rasmi ya uchaguzi, Kenyatta atazamiwa kushinda
-
Rais Uhuru Kenyatta
Wakenya wangali wanasuburi matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais wa marudio uliofanyika Alhamisi huku Uhuru Kenyatta akiwa bado anaongoza na akitazamiwa kutangazwa mshindi baada ya kinara wa upinzani Raila Odinga kususia uchaguzi huo.
Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) imetoa taarifa leo alasiri na kusema imepokea fomu za matokeo ya uchaguzi kutoka maeneo bunge 232 kati ya maeneo bunge 291. Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati amesema zoezi la kuchunguza fomu hizo lingali linaendeela.
Hadi kufikia leo mchana baada ya kuidhinisha matokeo ya majimbo 71 kati ya 291 Uhuru Kenyatta alikuwa amepta kura 2, 477, 878.
Wananchi wa Kenya Alkhamisi iliyopita walielekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa marudio wa urais kufuatia kutenguliwa ule wa awali uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Taarifa zinasema katika ghasia zilizoibuka tokea wakati wa uchaguzi huo wa Alhamisi watu tisa wameuawa.
Jana Ijumaa, Raila Odinga, kinara wa muungano wa NASA ambao umebadilishwa jina na kuwa Vuguvugu la Mageuzi (NRM) alidai kuwa kujitokeza idadi ndogo ya watu katika uchaguzi huo ni ishara tosha kuwa kulikuwa na uchakachuaji katika uchaguzi wa Agosti 8. Ameongeza kuwa atashinikiza uchaguzi mwingine ufanyike ndani ya siku 90.
Mahakama ya Juu ya Kenya ilitengua matokeo ya uchaguzi huo wa rais kwa hoja kwamba IEBC ilifanya baadhi ya makosa katika mchakato wa uchaguzi. Muungano wa upinzani uliwahimiza wafuasi wake kutoshiriki uchaguzi huo baada ya kiongozi wa muungano huo Raila Odinga kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.
Katika hatua nyingine, IEBC imetangaza kuakhirisha tena zoezi la upigaji kura lililotazamiwa hii leo, katika kaunti nne za Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya, ambazo ni ngome za NASA, ambako siku ya Alhamisi wakazi wake hawakupiga kura kwa sababu za kiusalama.