Kamanda wa jeshi la Burundi auawa kwa kupigwa risasi
-
Kanali Ikurakure
Kamanda mmoja wa jeshi la Burundi ameuawa kwa kupigwa risasi.
Kanali Darius Ikurakure ambaye alikuwa kamanda wa kikosi cha jeshi la Burundi katika eneo la Muzinda umbali wa kilomita 20 kutoka Bujumbura aliuawa jana kwa kupigwa risasi na askari mmoja. Askari huyo alitoweka baada ya kutekeleza mauaji hayo. Habari ya mauaji ya Kanali Darius Ikurakure imethibitishwa na afisa mmoja wa ngazi za juu katika jeshi la Burundi ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Wapinzani wa Burundi wanamtuhumu Kanali Darius Ikurakure kuwa alikuwa miongoni mwa wahusika wakuu wa ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo.
Hadi sasa jeshi la Burundi halijatangaza hatua yoyote kuhusu mauaji hayo.
Ghasia za sasa zimekuwa zikishuhudiwa nchini Burundi tangu Aprili mwaka jana wakati Rais wa sasa wa nchi hiyo alipotangaza kuwa atagombea kiti hicho kwa mara ya tatu.