Mahakama Kuu ya Liberia yasimamisha duru ya pili ya uchaguzi wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36108-mahakama_kuu_ya_liberia_yasimamisha_duru_ya_pili_ya_uchaguzi_wa_rais
Mahakama ya Juu nchini Liberia imesimamisha duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyotazamiwa kufanyika mapema wiki ijayo, kutokana na madai ya uchakachuaji na dosari chungu nzima katika uchaguzi wa Oktoba 10.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 02, 2017 04:06 UTC
  • Mahakama Kuu ya Liberia yasimamisha duru ya pili ya uchaguzi wa rais

Mahakama ya Juu nchini Liberia imesimamisha duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyotazamiwa kufanyika mapema wiki ijayo, kutokana na madai ya uchakachuaji na dosari chungu nzima katika uchaguzi wa Oktoba 10.

Mahakama hiyo imemtaka aliyewasilisha kesi hiyo ya kupinga matokeo ya urais kinara wa chama cha Liberty Charles Brumskine, na ambaye aliibuka wa tatu katika uchaguzi huo pamoja na Tume Taifa ya Uchaguzi NEC kuwasilisha katika mahakama hiyo nyaraka muhimu zinazohitaji kwa ajii ya kesi hiyo leo Alkhamisi. 

Mwenyekiti wa chama hicho Benjamin Sanvee amepongeza hatua hiyo ya Mahakama ya Juu na kusema kuwa: "Hii ni hatua kubwa ya kuelekea katika njia iliyo sahihi. Mahakama imezingatia uzito wa jambo hilo na imechukua hatua ya kulinda sheria na demokrasia."

Mwenyekiti wa NEC, Jerome Korkoya amekosoa vikali hatua hiyo akisisitiza kuwa, haoni haja ya Mahakama ya Juu kusimamisha maandalizi ya uchaguzi huo kukiwemo kuwapa mafunzo maafisa wa tume hiyo kwa ajili ya kujitayarisha kwa zoezi la duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

Rais anayeondoka wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf

Mwezi uliopita, Tume ya Uchaguzi nchini Liberia ilitangaza kuwa, mchezaji soka nyota wa zamani wa kimataifa Seneta George Weah na Makamu wa Rais Joseph Boakai watachuana katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais Novemba 7 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa NEC, asilimia 74 ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki zoezi hilo la kidemokrasia, ambapo Weah alipata asilimia 39 huku Boakai akipata asilimia 29 ya kura.