UN: Watu milioni 1.2 wakabiliwa na baa la njaa Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umesema watu milioni moja, laki mbili na elfu 50 wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na baa la njaa nchini Sudan Kusini.
Katie Rickard, mratibu wa kieneo wa shirika la kibinadamu la REACH lililotoa takwimu hizo leo Jumatatu kwa niaba ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Juba amesema idadi hiyo ni maradufu ya ile ya mwaka jana wakati kama huu akisisitiza kuwa, iwapo hatua za dharura hazichakuliwa, basi nchi hiyo itatumbukia katika janga la njaa kufikia mwaka ujao 2018.
Mpango wa Chakula wa Duniani WFP umesema watu laki moja wanakodolea macho kifo katika kaunti za Ayod na Greater Baggari kutokana na kusakamwa na hali mbaya ya njaa.
Kwa mujibu wa Idara Taifa ya Takwimu nchini Sudan Kusini, asilimia 56 ya raia wa nchi hiyo changa barani Afrika, sawa na watu milioni 6 wanakabiliwa na baa la njaa.

Hali hii ya njaa pamoja na machafuko yamesababisha maelfu ya raia wa Sudan Kusini waendelee kumiminika katika nchi jirani za Sudan na Uganda wakitafuta mahala salama pa kuishi na chakula.
Sudan Kusini ilitumbukia kwenye mgogoro mkubwa tangu Rais Salva Kiir alipomtuhumu makamu wake wa zamani Riek Machar kuwa alipanga njama za kumpindua mwezi Disemba 2013. Makumi ya maelfu ya watu wameshauawa na mamilioni ya wengine kupoteza makazi yao kutokana na machafuko yaliyoikumba nchini hiyo changa zaidi duniani.