UN yaonya tena: Sudan Kusini inakaribia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Sudan Kusini iko kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huku ghasia kati ya pande zinazohasimiana zikiongezeka.
"Hali nchini humo ni mbaya", amesema Nicholas Haysom, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), huku mvutano kati ya vikosi vinavyomuunga mkono na Rais Salva Kiir na vile vya Makamu wa Rais, Riek Machar ukiendelea kutokota.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, juhudi za kujadili makubaliano ya amani zingewezekana tu iwapo Kiir na Machar "wataweka masilahi ya taifa mbele ya maslahi yao wenyewe," na kuonya kwamba taarifa potofu na matamshi ya chuki yanachochea uhasama wa kikabila na ghasia zinazoongezeka ambazo zimewalazimisha makumi ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao.
Yapata wiki moja iliyopita, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) nchini Sudan Kusini ilitangaza kuwa, tangu mwishoni mwa mwezi uliopita, ghasia hizo zimewakosesha makazi watu 50,000, wakiwemo 10,000 ambao wamevuka mpaka na kuingia Ethiopia.
Sudan Kusini, nchi changa zaidi duniani, ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mara tu baada ya kujitenga na Sudan mwaka 2011, huku vikosi vilivyoungana na Kiir, vya kabila la Dinka, vikipigana na askari watiifu kwa Machar, kutoka kabila la Nuer.