Wananchi wa Somaliland washiriki uchaguzi wa rais, matokeo Ijumaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36386-wananchi_wa_somaliland_washiriki_uchaguzi_wa_rais_matokeo_ijumaa
Mamia ya maelfu ya wananchi wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Somaliland nchini Somalia wamejitokeza katika uchaguzi wa kumchagua rais wa tano wa eneo hilo, ambao unashuhudia ushindani mkali kati ya serikali na kambi ya upinzani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 14, 2017 03:53 UTC
  • Wananchi wa Somaliland washiriki uchaguzi wa rais, matokeo Ijumaa

Mamia ya maelfu ya wananchi wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Somaliland nchini Somalia wamejitokeza katika uchaguzi wa kumchagua rais wa tano wa eneo hilo, ambao unashuhudia ushindani mkali kati ya serikali na kambi ya upinzani.

Watu zaidi ya laki 7 wametimiza masharti ya kupiga kura katika eneo hilo lenye mamlaka ya ndani.

Uchaguzi huo ulifanyika jana Jumatatu chini ya ulinzi mkali, katika vituo zaidi ya 1,600 na matokeo yake rasmi yanatazamiwa kutolewa Ijumaa ijayo. 

Timu ya waangalizi 60 kutoka nchi 27 duniani wanafuatilia kwa karibu zoezi hilo la kidemokrasia katika eneo hilo la Pembe ya Afrika.

Ramani inayoonyesha eneo la Somaliland la Somalia

Muse Bihi Abdi, mgombea wa chama tawala cha Kulmiye anachuana vikali na mkuu wa mrengo wa upinzani Abdirahman Irro wa chama cha Wadani.

Mgombea mwengine wa uchaguzi wa rais katika eneo la Somaliland ni Faisal Ali Warabe, mwanasiasa mkongwe wa chama cha upinzani cha UCID.

Jamhuri ya Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 na kujitangazia mamlaka yake ya ndani huku mji mkuu ukiwa Hargeisa.

Hayo yalijiri baada ya kupinduliwa kwa aliyekuwa Rais wa Somalia Siad Barre mwaka huo huo.

Mji wa Hargeisa, makao makuu ya eneo la Somaliland