AU yasema Libya imegeuzwa kuwa kitovu cha soko la utumwa duniani
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika AU ametoa mwito kwa vyombo vya dola nchini Libya kuanzisha uchunguzi juu ya ripoti zinazosema kuwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ni kitovu cha biashara ya utumwa.
Akiongea jana Ijumaa, Alpha Conde ambaye pia ni rais wa Guinea amesema ni jambo la kusikitisha kuona vijana wa Kiafrika wanapigwa mnada hadharani kama bidhaa, baadhi yao wakiuzwa kwa kiasi cha dola 400 za Marekani.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, aghalabu ya vijana hao wa Kiafrika wanaouzwa katika masoko ya watumwa nchini Libya wanatokea nchi za Mali, Niger, Nigeria na Gambia
Septemba mwaka huu, ripoti iliyotolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na taasisi ya Walk Free ilisema kuwa, watu zaidi ya milioni 40 wakiwemo watoto wadogo hususan wenye asili ya Afrika, walikuwa wahanga wa utumwa mamboleo katika mwaka uliopita wa 2016.
Kwa mujibu wa Shirika la Wahajiri Duniani IOM, watu wanaofanya biashara haramu ya magendo ya wahajiri wanatengeneza faida ya dola bilioni 35 za Marekani kila mwaka nchini LIbya.