Iran: Afrika isigeuzwe kimbilio la magenge ya kigaidi na ukufurishaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36745-iran_afrika_isigeuzwe_kimbilio_la_magenge_ya_kigaidi_na_ukufurishaji
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia udharura wa kufanyika jitihada za kuzuia bara la Afrika kugeuka kuwa kimbilio na kitovu cha magenge ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu ada, kufuatia kusambaratishwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika nchi za Syria na Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 24, 2017 12:25 UTC
  • Iran: Afrika isigeuzwe kimbilio la magenge ya kigaidi na ukufurishaji

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia udharura wa kufanyika jitihada za kuzuia bara la Afrika kugeuka kuwa kimbilio na kitovu cha magenge ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu ada, kufuatia kusambaratishwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika nchi za Syria na Iraq.

Eshaq Jahangiri aliyasema hayo jana Alkhamisi mjini Tunis katika mazungumzo yake na Sabri Bachtobji, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia. Jahangiri alifanya safari fupi nchini Tunisia kabla ya kuelekea Bolivia, alikoenda kushiriki Mkutano wa Nchi Zinazouza Gesi (GECF).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amebainisha kuwa: "Kutokana na ukweli kwamba genge la Daesh limesambaratishwa katika nchi za Iraq na Syria, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za makusudi kuhakikisha kuwa mabaki ya kundi hilo hayazagai katika nchi za Afrika."

Kusambaratika kwa Daesh (ISIS)

Kwengineko katika mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, Eshaq Jahangiri ametoa mwito wa kutumiwa fursa na majukwaa yote kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Tunis.

Kwa upande wake, Sabri Bachtobji, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia amesema nchi yake ina hamu ya kuupeleka uhusiano na Iran katika hatua ya juu, huku akisisitiza umuhimu wa kufanyika mkutano hivi karibuni wa Kamisheni ya Pamoja ya Uchumi ya nchi mbili hizi.