Kenyatta amualika Odinga katika sherehe za kuapishwa kwake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36765-kenyatta_amualika_odinga_katika_sherehe_za_kuapishwa_kwake
Rais Uhuru Kenyatta amemualika 'ndugu yake' Raila Odinga katika sherehe za kuapishwa kwake zikatazofanyika katika mji mkuu Nairobi Jumanne ijayo ya Novemba 28.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 25, 2017 00:52 UTC
  • Kenyatta amualika Odinga katika sherehe za kuapishwa kwake

Rais Uhuru Kenyatta amemualika 'ndugu yake' Raila Odinga katika sherehe za kuapishwa kwake zikatazofanyika katika mji mkuu Nairobi Jumanne ijayo ya Novemba 28.

Joseph Kinyua, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Kumuapisha Rais jana Ijumaa aliwaambia waandishi wa habari kwamba, Odinga ambaye ni kinara wa muungano wa upinzani NASA pamoja na wagombea wengine wa kiti cha rais katika uchaguzi wa Agosti 8 na uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 wametumiwa barua za mualiko kwa ajili ya kuhudhuria hafla ya kumuapisha Kenyatta.

Hata hivyo ametahadharisha kuhusu mpango wowote wa wapinzani wa kufanya sherehe mbadala siku hiyo ya kuapishwa Rais Kenyatta kuhudumu kwa muhula wake wa pili na wa mwisho wa miaka mitano.

Kumekuwa na tetesi hususan katika mitandao ya kijamii kwamba mrengo wa NASA unapanga kumuapisha Odinga katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi Jumanne ijayo wakati ambapo Rais Kenyatta atakuwa anaapishwa katika Uwanja wa Taifa wa Kasarani jijini humo.

Majaji wa Mahakama ya Juu Kenya

Maandalizi ya kumuapisha Kenyatta yanafanyika baada ya Mahakama ya Kilele nchini Kenya kutupilia mbali kesi mbili zilizokuwa zimewasilishwa kupinga uchaguzi wa rais wa marudio wa Oktoba 26 uliosusiwa na Odinga, na hivyo kuidhinisha ushindi wa Uhuru Kenyatta.

Watu kadhaa waliuawa kufuatia ghasia zilizoshuhudiwa katika maeneo mbali mbali ya Kenya, baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Juu.