Al Bashir: Marekani ina mpango wa kuigawa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36787-al_bashir_marekani_ina_mpango_wa_kuigawa_sudan
Rais Omar al Bashir wa Sudan amesema kuwa mashinikizo na njama za Marekani ndivyo vilivyopelekea kugawanywa Sudan katika nchi mbili na kwamba Washington ina mpango wa kuigawa zaidi Sudan katika nchi tano tofauti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 25, 2017 12:44 UTC
  • Al Bashir: Marekani ina mpango wa kuigawa Sudan

Rais Omar al Bashir wa Sudan amesema kuwa mashinikizo na njama za Marekani ndivyo vilivyopelekea kugawanywa Sudan katika nchi mbili na kwamba Washington ina mpango wa kuigawa zaidi Sudan katika nchi tano tofauti.

Rais wa Sudan amesema leo katika mahojiano yake na shirika la habari la Sputnik la Russia kwamba, Marekani imezidisha mashinikizo na njama dhidi ya nchi yake na kwamba mambo hayo mawili ndiyo sababu ya kugawanywa Sudan na kujitenga Sudan Kusini.

Ameongeza kuwa, Khartoum ina taarifa za kiintelijensia zinazothibitisha kuwa Marekani inafanya mikakati ya kuigawa Sudan katika nchi tano na kwamba Washington inahusika na uharibu mkubwa unaoshuhudiwa katika nchi za Afghanistan, Iraq, Syria na Yemen na kugawanyika kwa Sudan.

Matamshi hayo ya Rais wa Sudan yametolewa baada ya kuzimwa njama za Marekani na washirika wake za kutaka kuzigawa nchi kadhaa za Kiislamu ikiwemo Syria na Iraq. Jaribio la karibuni kabisa la njama hizo za Marekani zinazofanyika kwa kutumia vibaraka wake ni kura ya maoni ya kutaka kujitenga eneo la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq ambayo imezimwa kutokana na kuwa macho viongozi wa Iraq na washirika wa nchi hiyo hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.