Nov 28, 2017 07:39 UTC
  • Rais wa Ufaransa akaribishwa Burkina Faso kwa shambulizi la guruneti

Kwa akali watu watatu wamejeruhiwa katika shambulizi la guruneti nchini Burkina Faso, lililofanyika masaa machache kabla ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuanza ziara ya kuitembelea nchi hiyo ya Kiafrika.

Duru za usalama zimesema watu wawili waliokuwa juu ya pikipiki huku wakiwa wamefunika nyuso zao walilirushia guruneti gari lililokuwa limewabeba wanajeshi wa Ufaransa karibu na lango la kambi ya Kikosi Maalumu cha Ufaransa, ambapo raia watatu wamejeruhiwa.

Masaa matatu baada ya hujuma hiyo ya jana Jumatatu, Rais Macron aliwasili katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, kuanza safari ya kuitembelea nchi hiyo pamoja na Ivory Coast na Ghana. Alipokewa na mwenyeji wake, Rais Roch Marc Christian Kabore.

Burkina Faso kama zilivyo nchi nyingine za magharibi mwa Afrika, imekuwa ikilengwa mara kwa mara kwa mashambulizi ya makundi ya kitakfiri na yenye misimamo mikali.

Usalama waimarishwa Ougadougou baada ya hujuma ya guruneti

 

Mwezi Agosti mwaka huu, genge la watu waliokuwa na silaha liliua raia wasiopungua 17 na kujeruhi wengine 8 baada ya kuvamia mgahawa mmoja katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou.

Aidha watu 30 waliuawa Januari mwaka jana baada ya magaidi wa kundi la kiwahabi la AQIM kuvamia mgahawa na hoteli mmoja mjini Ouagadougou   

Tags