UN yasisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo DRC
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuna udharura wa kufanyika mazungumzo baina ya wanasiasa wa nchi hiyo kwa shabaha ya kukomesha hitilafu za ndani.
Maman Sidikou ameashiria kwamba uchaguzi wa rais ulipaswa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Congo DR na kuongeza kuwa, mchakato wa uchaguzi huo umesimama kwa sasa, hivyo kuna udharura wa kuwepo mazungumzo kati ya wanasiasa wa Congo.
Maman Sidikou ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kadiri wakati wa uchaguzi mkuu nchini Congo DR unavyokaribia mivutano na ghasia za kisiasa zinaongezeka zaidi nchini humo. Amesema kuna vizuizi vikuu ambavyo vinapaswa kuondolewa kabla ya uchaguzi wa rais nchini Congo.
Amesisitiza kuwa kuna uwezekano wa kutokea ghasia na machafuko makubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iwapo hitilafu zilizopo kati ya wanasiasa wa nchi hiyo hazitatatuliwa.