Afrika Kusini na Morocco kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37133-afrika_kusini_na_morocco_kuhuisha_uhusiano_wao_wa_kidiplomasia
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema nchi hiyo itafufua uhusiano wa kidiplomasia na Morocco, baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja tangu nchi hiyo ya Kiarabu imuondoe balozi wake mjini Pretoria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 03, 2017 11:03 UTC
  • Afrika Kusini na Morocco kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema nchi hiyo itafufua uhusiano wa kidiplomasia na Morocco, baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja tangu nchi hiyo ya Kiarabu imuondoe balozi wake mjini Pretoria.

Zuma amesema hayo katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti la City Press na kuongeza kuwa, Morocco ni nchi ya Kiafrika na kuna haja ya kuimarisha uhusiano nayo.

Rais wa Afrika Kusini amebainisha kuwa: "Sisi hatukuwa na tatizo na Morocco, ni wao waliokuwa wa kwanza kukata uhusiano wa kidiplomasia na sisi. Wameonelea kuwa, licha ya kwamba tunatofautiana katika kadhia ya Sahara Magharibi, lakini kuna umuhimu wa nchi mbili hizi kuwa na uhusiano."

Zuma na Mfalme Mohammed VI wa Morocco

Zuma alikutana na Mfalme VI wa Morocco wiki iliyopita, pambizoni mwa mkutano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya katika mji wa Abidjan nchini Ivory Coast.

AU iliafiki rasmi kujiunga tena Morocco na jumuiya hiyo katika mkutano wa 28 wa umoja huo uliofanyika mwezi Januari mwaka huu baada ya kupita miongo mitatu. Morocco ilijiondoa katika Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika mwaka 1976.