Kwa siku watu 15000 wanalazimika kuwa wakimbizi wa ndani barani Afrika
Vita, ukatili na unyanyasaji unaoendelea kushuhudiwa katika nchi nyingi za Afrika vimesababisha wastani wa watu 15 elfu kuwa wakimbizi wa ndani kila siku, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2017.
Ripoti iliyotolewa na mashirika ya Internal Displacement Monitoring Centre (IDMC) na Norwegian Refugee Council (NRC) imebainisha kuwa, Waafrika milioni mbili na laki saba wamelazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi zao katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.
Ripoti hiyo imesema idadi hiyo haijumuishi raia wa Afrika waliokimbia nje ya nchi kuwa wakimbizi au kutafuta hifadhi. Kufikia mwishoni mwa mwaka jana 2016, watu milioni 12 na laki sita walikuwa wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani (IDP's).
Ripoti iliyotolewa Jumatano ya leo na mashirika hayo imeonyesha kuwa, aghalabu ya wakimbizi hao wa ndani ya nchi ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria na Sudan Kusini.
Watu milioni 1 wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani Kongo DR katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na mwaka mzima wa 2016; huku watu laki mbili wakifurushwa makwao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, watu milioni 65 na laki sita walilazimika kuwa wakimbizi kote duniani hadi kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2016.