Sudan Kusini yahitaji misaada ya kibinadamu ya dola bilioni 1.7
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37581-sudan_kusini_yahitaji_misaada_ya_kibinadamu_ya_dola_bilioni_1.7
Sudan Kusini inahitaji misaada ya kibinadamu ya dola bilioni 1.7 katika mwaka ujao wa 2018 ili kuwasaidia raia wa nchi hiyo wapatao milioni 6; idadi ambayo ni nusu ya jamii ya nchi hiyo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 13, 2017 23:43 UTC
  • Sudan Kusini yahitaji misaada ya kibinadamu ya dola bilioni 1.7

Sudan Kusini inahitaji misaada ya kibinadamu ya dola bilioni 1.7 katika mwaka ujao wa 2018 ili kuwasaidia raia wa nchi hiyo wapatao milioni 6; idadi ambayo ni nusu ya jamii ya nchi hiyo.

Msaada huo unahitajika huko Sudan Kusini ili kukabiliana na athari za vita, njaa na kuyumba hali ya uchumi wa nchi hiyo. Hayo yameelezwa na serikali na Umoja wa Mataifa hapo jana.

Raia wa Sudan Kusini wakiwa katika moja ya kambi za hifadhi 

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013; miaka miwili baada ya kupata uhuru kutoka Sudan. Theluthi moja ya jamii ya Wasudani Kusini wapatao milioni 12 wamekimbia makazi yao kutokana na vita hivyo. Mzozo huo ulisababishwa na hali ya mvutano uliojitokeza kati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na aliyekuwa Makamu wake Riek Machar; ambaye hivi sasa yuko Afrika Kusini.

Alain Noudehou Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema kuwa wanatoa wito wa kupatiwa dola bilioni 1.72 ili kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu na kuwalinda raia wa Sudan Kusini milioni sita ambao wanahitaji misaada ya haraka.