Uturuki kuujenga upya mji 'wake' wa kale wa bandari huko Sudan
Sudan imesema kuwa Uturuki itaujenga upya mji wa bandari ulioharibiwa wakati wa zama za Othmaniya unaopatikana katika Ukanda wa pwani ya Sudan huko katika Bahari Nyekundu, ikiwa ni katika juhudi za Ankara za kupanua mahusiano yake ya kijeshi na kiuchumi barani Afrika.
Ibrahim Ghandour, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan alitangaza habari hiyo jana Jumanne akisema kuwa, ujenzi huo mpya katika kisiwa cha Suakin kilichoko kaskazini mashariki mwa Sudan uliafikiwa kufuatia ziara ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki katika bandari hiyo ya kale mapema juzi.

Rais wa Uturuki ambaye alikuwa ziarani Khartoum mji mkuu wa Sudan ikiwa ni sehemu ya safari yake ya siku tatu barani Afrika, juzi alisema kuwa Rais wa Sudan Omar al Bashir amekubali kuikabidhi Ankara kwa muda kisiwa cha Suakini kwa ajili ya kukijenga upya lengo likiwa ni kukifanya kisiwa hicho kuwa eneo la utalii na kituo kwa wale wote wanaotaka kufanya umrah au hija ndogo zaidi katika maeneo matakatifu nchini Saudi Arabia kutokea Uturuki. Kisiwa hicho cha Suakini ambacho kilihesabiwa kama kitovu cha starehe katika Bahari Nyekundu; kilikuwa bandari kuu ya Sudan wakati ilipokuwa chini ya utawala wa Othmaniya, lakini kisiwa hicho kilikuwa hakitumiki katika kipindi cha karne moja iliyopita kufuatia ujenzi wa bandari ya Sudan umbali wa kilomita 60 kwa upande wa kaskazini.