Watetezi wa haki za binadamu Misri walaani kunyongwa washukiwa wa ugaidi
Mashirika saba ya kutetea haki za binadamu nchini Misri yamekosoa vikali hatua ya Misri kuwanyonga watu 15 waliopatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi yaliyoua askari usalama huko kaskazini mwa Peninsula ya Sinai.
Taarifa ya mashirika hayo yakiwemo Egyptian Initiative for Personal Rights, Nadim Center Against Violence and Torture na Egyptian Commission for Rights and Freedoms imesema mchakato wa kisheria hadi kufikia uamuzi wa kuwanyonga watu hao ulizungukwa na kasoro na mapungufu mengi, na kwamba mmoja wa watuhumiwa hao alikuwa na majeraja, ishara kwamba aliteswa kabla ya kunyongwa.
Kadhalika ripoti imesema familia za watu hao zilikatazwa kuwaona wapendwa wao siku hiyo ya kutekelezwa hukumu hiyo, kama inavyoanisha sheria ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Mahakama ya kijeshi ya Misri iliwapata 15 hao na hatia ya kuua maafisa usalama katika kituo cha upekuzi mnamo Agosti 15 mwaka 2013, siku moja baada ya waandamanaji 600 wafuasi wa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo, Mohammed Morsi kuuawa na maafisa usalama mjini Cairo.
Watu hao walinyongwa katika jela mbili za Borj al-Arab na Wadi al-Natroun zilizoko kaskazini mwa Misri mapema Jumanne iliyopita, operesheni inayooenakana kuwa kubwa zaidi kuwahi kufanywa katika siku moja nchini Misri tangu Abdul Fattah al-Sisi alipochukua madaraka nchini humo mwaka 2014.
Wapiganaji wa makundi ya kigaidi na kiwahabi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.