Ethiopia yailaumu Saudia kwa kuwanyanyasa na kuwaadhibu Waethiopia waliofukuzwa nchini humo
Serikali ya Ethiopia imeulaumu utawala wa Saudi Arabia kwa sababu ya vitendo vya unyanyasaji na vya kuwaadhibu maelfu ya raia wa Ethiopia waliofukuzwa nchini Saudia.
Serikali ya Addis Ababa imetangaza kuwa maelfu ya raia wa nchi hiyo ambao wamefukuzwa kwa wingi na kwa umati nchini Saudi Arabia kupitia mpango mpya uliotekelezwa hivi karibuni na viongozi wa utawala wa Riyadh wamefanyiwa vitendo vya unyanyasaji na haki zao za msingi zimekiukwa.
Baada ya kurejeshwa nchini kwao, Waethiopia hao wamesimulia kuwa walipigwa na kutukanwa huko nchini Saudia, wakaibiwa vitu vyao na pia kuwekwa kwenye jela na mahabusu chafu zilizofurika watu.

Serikali ya Ethiopia imeeleza kuwa kuanzia katikati ya mwezi uliopita wa Novemba hadi sasa, zaidi raia 14,000 wa nchi hiyo wamefukuzwa nchini Saudi Arabia, hata hivyo kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa ya Uhajiri takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu waliohamishwa kwa nguvu nchini Saudia inafikia elfu 98.
Maafisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch nao pia wameeleza kuhusiana na suala hilo kwamba katika mahojiano waliyowafanyia makumi ya raia wa kigeni waliofukuzwa nchini Saudia mwaka 2014, wengi wao walisimulia kuhusu hali mbaya ya mazingira ya mahabusu, kuhamishwa kwa nguvu pamoja na kushambuliwa, kupigwa na kutusiwa na askari wa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.../