Misri yawanyonga washukiwa wengine wanne wa ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38429-misri_yawanyonga_washukiwa_wengine_wanne_wa_ugaidi
Mamlaka ya Magereza ya Misri imetekeleza hukumu ya kuwanyonga watu watano wakiwemo wanne waliopatikana na hatia ya kutekeleza mashambulizi ya bomu yalioua maafisa usalama miaka miwili iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2018 10:53 UTC
  • Misri yawanyonga washukiwa wengine wanne wa ugaidi

Mamlaka ya Magereza ya Misri imetekeleza hukumu ya kuwanyonga watu watano wakiwemo wanne waliopatikana na hatia ya kutekeleza mashambulizi ya bomu yalioua maafisa usalama miaka miwili iliyopita.

Hukumu hizo za Jumanne ya leo zimetekelezwa katika gereza la Burj al-Arab, magharibi mwa mji wa pwani wa Alexandria. 

Wanne hao wanasemekana kuhusika katika shambulizi la bomu dhidi ya kituo cha mafunzo ya kijeshi katika mji wa Kafr al-Sheikh eneo la Nile Delta, katika ghasia zilizoibuka baada ya kuondolewa mamlakani Mohammad Mursi, rais wa zamani wa nchi hiyo.

Kitanzi

Hii ni katika hali ambayo, mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo yakiwemo ya Egyptian Initiative for Personal Rights, Nadim Center Against Violence and Torture na Egyptian Commission for Rights and Freedoms yalikosoa vikali mchakato wa kisheria hadi kufikia uamuzi wa kuwanyonga watu 15 katika hukumu iliyotolewa mwishoni mwa mwezi uliopita.

Disemba 26 mwaka uliomalizika, Misri iliwanyonga watu wengine 15 waliopatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi yaliyoua askari usalama huko kaskazini mwa Peninsula ya Sinai.