Wanamgambo 23 wa al Shabab wauliwa na askari wa Somalia
Kwa akali wanachama 23 wa kundi la kigaidi la ash-Shabab la Somalia wameuliwa na askari wa serikali ya nchi hiyo.
Maafisa wa serikali ya Mogadishui wametangaza kuwa, wanamgambo hao wa ash-Shabab wameuawa katika mapigano makali kati yao na askari wa serikali. Kwa mujibu wa ripoti hiyo mapigano hayo yamejiri katika mji wa Galmudug nchini Somalia na kwamba wapiganaji wengine 22 wa ash Shabab wamejeruhiwa. Muhammad Aden Osman mmoja wa viongozi wa eneo hilo amenukuliwa akisema kuwa, mapigano hayo yaliyoibuka jana yameendelea hadi leo na kwamba ripoti zinaeleza kuwa askari wa serikali wamepata ushindi dhidi ya magaidi hao. Osman ameongeza kuwa, mapigano ya hapo jana yaliyojiri kwa lengo la kuwatia mbaroni wapiganaji wa kundi hilo waliokuwa wamekimbilia katika mji huo, yalifanikisha pia kukamatwa silaha na zana za kijeshi zilizokuwa zikitumiwa na wanamgambo hao.