Jeshi la Ivory Coast latangaza utayari wa kushirikiana na serikali
Mkuu wa majeshi ya Ivory Coast ametangaza utayari wa jeshi hilo wa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo.
Meja Jenerali Ahmad Sekou Touré amesema kupitia ujumbe aliotoa kwa wananchi kwamba ana matumaini mwaka 2018 jeshi la nchi hiyo litaweza kutekeleza wajibu wake na kufidia mapungufu yanayohusiana na matukio ya mwaka uliopita.
Mkuu wa majeshi ya Ivory Coast aidha amewaomba radhi wananchi kutokana na machafuko yaliyojiri baada ya uasi uliotokea nchini humo.
Jenerali Sekou Touré aliteuliwa kushika wadhifa huo mwezi Januari mwaka 2017 baada ya uasi wa wanajeshi lakini hakuweza kuzuia kuendelea uasi huo mnamo mwezi Mei mwaka huo.
Malalamiko yaliyoanzishwa na waasi wa zamani ambao walijiunga na jeshi la Ivory Coast, ya kudai marupurupu makubwa yaliiyumbisha serikali ya Abidjan katika kipindi cha miezi ya Januari na Mei mwaka uliopita.
Askari wapatao elfu moja waliihama nchi mwezi uliopita wa Desemba katika mageuzi yaliyofanywa jeshini.
Hadi mwaka 2011, Ivory Coast ilikuwa ikishuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe; lakini baada ya kufikiwa makubaliano ya amani wanamgambo wengi wa makundi ya waasi walijiunga na jeshi, ambapo kwa mujibu wa viongozi wa serikali ndio waliohusika na uasi uliotokea nchini humo mwaka 2017.../