Jeshi: Vijana 13 wauawa kwa kufyatuliwa risasi kusini mwa Senegal
Jeshi la Senegal limetangaza habari ya kuuawa vijana 13 kwa kufyatuliwa risasi na genge la wabeba silaha, kusini mwa nchi.
Msemaji wa jeshi, Abdoul Ndiaye amesema wavamizi hao waliwashambulia kwa risasi vijana waliokuwa wakitema kuni jana Jumamosi katika mji wa Borofaye, eneo la kusini la Casamance, yapata kilomita 10 kutoka mpaka wa nchi hiyo na Guinea Bissau.
Kundi linaloshinikiza kujitenga eneo hilo la Movement of Democratic Forces for Casamance (MFDC) limekuwa likiendeleza harakati zake tangu 1982.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, Rais Macky Sall wa Senegal alisisitiza kwamba, nchi yake inatambua na kuunga mkono kikosi cha Kundi la Nchi 5 za Sahel Afrika katika vita dhidi ya ugaidi na kukabiliana na ukosefu wa usalama.
Alisisitiza kuwa, nchi hiyo itafanya kila iwezalo kwa ajili ya kufikiwa malengo ya kundi la nchi hizo, linaloundwa na Senegal, Burkina Faso, Mauritania, Niger na Chad.
Eneo la Sahel Magharibi limekuwa likilengwa na mashambulio ya makundi ya kufurutu ada na ya kigaidi lilikiwemo kundi la Boko Haram la Nigeria.