Operesheni ya kijeshi ya jeshi la Libya yamalizika katika mpaka wa Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38701-operesheni_ya_kijeshi_ya_jeshi_la_libya_yamalizika_katika_mpaka_wa_tunisia
Baraza la uongozi la serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya limetangaza habari ya kumalizika operesheni za kijeshi za nchi hiyo katika eneo la Abu Kammash karibu na kivuko cha Ras Jdir kwenye mpaka wa Libya na Tunisia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2018 01:15 UTC
  • Operesheni ya kijeshi ya jeshi la Libya yamalizika katika mpaka wa Tunisia

Baraza la uongozi la serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya limetangaza habari ya kumalizika operesheni za kijeshi za nchi hiyo katika eneo la Abu Kammash karibu na kivuko cha Ras Jdir kwenye mpaka wa Libya na Tunisia.

Shirika la habari la Fars limenukuu taarifa ya jana Jumatatu ya baraza hilo ikisema kuwa tayari taasisi za serikali zimetakiwa kwenda kwenye kivuko cha Ras Jadir kuendesha shughuli zao za kiserikali na kusimamia usalama katika eneo lote la mpaka wa Libya na Tunisia. Hata hivyo taarifa hiyo imesema, hii haina maana kwamba vitendo vya uhalifu vimemalizika kikamilifu, bali duru za usalama zitaendelea kuwasaka na kuwashughulikia wahalifu na wavunjaji wote wa amani katika maeneo hayo.

Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya

 

Hivi karibuni makundi yenye silaha yalivamia kivuko cha mpakani cha Ras Jdir na kupelekea kivuko hicho kufungwa kabla ya askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya kutumwa na kufanikiwa kurejesha amani.

Viongozi wa Libya  wamesema, lengo la shambulizi hilo la watu wenye silaha lilikuwa ni kuudhibiti mpaka wa Libya na Tunisia na kuwafukuza askari watiifu kwa serikali ya umoja wa kitaifa katika kivuko hicho.

Libya haijawahi kushuhudia utulivu na amani tangu mwaka 2011, wakati Marekani na waitifaki wake katika shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO walipoivamia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kufanya uharibifu mkubwa katika kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi. Baada ya hapo mabeberu wa nchi za Magharibi waliitelekeza Libya na kuacha silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa makundi hasimu ambayo kila moja hadi leo hii linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo.