Wahajiri 100 wahofiwa kufa maji katika Bahari ya Mediterranean
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38773-wahajiri_100_wahofiwa_kufa_maji_katika_bahari_ya_mediterranean
Jeshi la Majini la Libya limetangaza kuwa yumkini wahajiri 100 waliotoweka katika ajali ya boti katika Bahari ya Mediterranean wakiwa safarini kulekea Ulaya, wamekufa maji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 10, 2018 12:26 UTC
  • Wahajiri 100 wahofiwa kufa maji katika Bahari ya Mediterranean

Jeshi la Majini la Libya limetangaza kuwa yumkini wahajiri 100 waliotoweka katika ajali ya boti katika Bahari ya Mediterranean wakiwa safarini kulekea Ulaya, wamekufa maji.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo leo Jumatano imesema wahajiri hao wanaohofiwa kuaga dunia walikuwa katika boti moja hafifu ya plastiki na kwamba wengine 279 waliokuwa kwenye boti tofauti wameokolewa katika ajali hiyo iliyotokea katika pwani ya mji wa magharibi wa Khoms, huku wengine wakiokolewa karibu na mji wa Zawiya.

Miongoni mwa waliokolewa ni wanawake 19 na watoto wadogo 17.

Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) Jumatatu iliyopita lilitangaza kuwa, boti iliyokuwa imewabeba wahajiri 150 lilizama katika pwani ya Libya baada ya kupata hitilafu ambapo wahajiri 64 walifariki dunia. 

Operesheni ya kuwaokoa wahajiri wa Kiafrika

Kwa mujibu wa IOM, zaidi ya wakimbizi elfu tatu waliaga dunia mwaka jana wakijaribu kufika Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania, vifo ambavyo vingi vilitokea katika njia ya bahari kutoka Libya kuelekea Italia, ikilinganishwa na elfu tano mwaka juzi.

Akthari ya wahajiri hao ni raia wa nchi za Kiafrika ambao wanataraji kupata maisha mazuri na ajira huko barani Ulaya.