Jan 17, 2018 08:23 UTC
  • Mahakama ya Ufaransa yawaachia huru askari waliowanajisi watoto Bangui

Mahakama moja nchini Ufaransa imetangaza kuhitimisha faili la tuhuma za askari wa nchi hiyo waliowanajisi watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa madai ya kutokuwepo ushahidi wa kutosha.

Jumanne ya jana mahakama ya Ufaransa ilidai kwamba, hakuna nyaraka wala ushahidi wa kutosha kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili askari wake walioko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya mwamvuli wa kikosi cha Sangaris kwa kuhusika na kuwabaka na kuwadhalilisha kijinsia watoto wadogo wa taifa hilo.

Askari wa Ufaransa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Itakumbukwa kuwa mwaka 2015 askari kadhaa wa Ufaransa walituhumiwa kuhusika na vitendo hivyo baada ya watoto kadhaa kutoa ushahidi kwamba walikumbwa na udhalilishaji wa askari hao. Kwa mujibu wa watoto hao, askari wa Ufaransa walikuwa wakiwarubuni watoto wadogo wa jinsia tofauti kwa kuwapa mkate au bisikuti na kisha kuwafanyia ukatili huo.

Watoto wadogo wa nchi hiyo hawako salama kutokana na askari wa Ufaransa

Kufuatia hali hiyo raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliandamana wakitaka askari hao wachukuliwe hatua kwa kushitakiwa na mahakama za nchi hiyo, ingawa serikali ya Paris iliwarejesha askari hao na kuahidi kuwashitaki katika mahakama zake, kitendo ambacho kilitafsiriwa kama mchezo wa kisiasa. Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko mwaka 2013 kufuatia uingiliaji wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Ufaransa.

Tags