Wimbi la utekaji nyara watu laendelea kuikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Watu wengine watatu akiwemo askofu mmoja wametekwa nyara mashariki mwa Jamhuri ya Kidemkorasia ya Kongo.
Mkutano wa kitaifa wa Uaskofu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umetangaza kuwa Askofu Robert Masinda pamoja na wahandisi wawili wa kilimo walitekwa nyara siku ya Jumatatu usiku katika mji wa Beni mkoani Kivu Kaskazini.
Gavana wa mji wa Beni amethibitisha habari hiyo lakini amesema mbali na askofu mmoja watu wengine wanne wametekwa nyara katika tukio hilo.
Mkoa wa Kivu Kaskazini ambao ni kitovu cha harakati za makumi ya makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha umekuwa kila mara ukishuhudia matukio ya utekaji nyara raia.
Hivi karibuni pia watu wapatao 12 walitekwa nyara karibu na eneo la Beni na wanamgambo wa kundi la waasi wa Uganda la ADF.
Mnamo mwezi Julai mwaka uliopita wa 2017 pia maaskofu wawili wa Dayosisi ya Beni-Butembo walitekwa nyara na wanamgambo wasiojulikana.../