MapiganoTanganyika na Kivu Kusini nchini DRC yapelekea watoto 800,000 kukosa makao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39479-mapiganotanganyika_na_kivu_kusini_nchini_drc_yapelekea_watoto_800_000_kukosa_makao
Watu zaidi ya millioni moja , wakiwemo watoto 800,000 wamelazimika kuyahama makao yao kutokana na ghasia za kikabila pamoja na mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha pamoja na waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jan 26, 2018 00:11 UTC
  • MapiganoTanganyika na Kivu Kusini  nchini DRC yapelekea watoto 800,000 kukosa makao

Watu zaidi ya millioni moja , wakiwemo watoto 800,000 wamelazimika kuyahama makao yao kutokana na ghasia za kikabila pamoja na mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha pamoja na waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC.

Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto UNICEF, ambalo linasema  vurugu hizo nyingi ziko katika mikoa ya Kivu Kusini na Tanganyika.

UNICEF imeongeza kuwa watoto mashariki mwa DRC sio tu wanafanyiwa ukatili wa kingono lakini pia husajiliwa katika makundi yenye silaha kwa minajili ya kupigana  vita.

UNICEF na washirika wake wameorodhesha visa zaidi ya 800 mashariki mwa DRC vya ukatili wa kingono kwa wototo japo  idadi kamili ya visa hivyo inaaminiwa kuwa kubwa zaidi.

Takwimu za hivi karibuni za UNICEF zinaonyesha katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita, watoto Zaidi ya 3,000 wameingizwa katika makundi ya wanamgambo pamoja na makundi mengine yenye silaha.

Rais Joseph Kabila wa DRC

Hofu ya UNICEF ni mapigano yalivyoathiri afya pamoja na lishe ya watoto na hivyo sio tu inasaidia watu wasio na makazi lakini pia imeomba  msaada wa dola millioni 65 kama sehemu yake ya mpango wa dharura wa kusaidia mikoa  ya Tanganyika na Kivu kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Usalama umekuwa ukizirota kote DRC tokea Disemba mwaka 2016 wakati Rais Joseph Kabila alipokataa kuachia ngazi pamoja na kuwa muhula wake ulikuwa umemalizika kikatiba.

Eneo la Mashariki mwa DRC kwa miongo kadhaa limekuwa kitovu cha mapigano kutokana na utajiri wake wa madini ambayo aghalabu yanaporwa na mashirika ya Ulaya na Marekani.