Uchumi wa Bara Afrika watazamiwa kustawi kwa kasi mwaka 2018
-
Kiwanda cha kutegeneza magari nchini Kenya
Uchumi wa bara Afrika unatazamiwa kustawi kwa asilimia 3.5 mwaka huu wa 2018 hilo likuwa ni ongezeko la 0.3 kutoka mwaka 2017, amesema afisa wa Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kiuchumi ya Afrika Bi.Vera Songwe ameyasema hayo Alhamisi kwenye mkutano wa kilele wa 30 wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia. Amebaini kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa mwaka huu na mwaka kesho inatarajiwa kufikia asilimia 3.5 na asilimia 3.7 mtawalia.
Songwe amesema ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa mahitaji ya ndani na bei ya bidhaa. Katika baadhi ya nchi za Afrika, uzalishaji wa mafuta umeongezeka tena, ufufukaji wa uchumi nchini Misri, Nigeria na Afrika Kusini pia umechangia ukuaji wa uchumi wa bara la Afrika.
Ameongeza kuwa nchi za Afrika bado zinakabiliwa na masuala ya umaskini na baa la njaa. Aidha amesema ingawa umasikini unaedelea kupungua barani Afrika bado kiwango cha umasikini ni kikubwa katika bara hilo. Ametowa wito wa kuendelezwa mageuzi ya kimuundo ili kuimarisha usimamizi wa uchumi na kuhimiza mafungamano ya nchi za Afrika.