Barua ya Trump kwa viongozi wa nchi za Kiafrika
Katika barua aliyowaandikia viongozi wa nchi za Afrika Rais Donald Trump wa Marekani amedai kwamba, anawaheshimu sana watu wa bara hilo.
Kadhalika pambizoni mwa kikao cha mjini Davos, Uswisi, na akizungumza na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Trump alimtaka rais huyo kufikisha hisia zake za dhati kwa viongozi wengine wa nchi za bara hilo. Hilo linajiri katika hali ambayo, katikati ya mwezi huu unaomalizika wa Januari, Trump alitoa matamshi machafu sana kwa kuzitaja nchi za Haiti, El Salvador na za Afrika kuwa ni 'shimo la kinyesi' huku akitaka kuzuiwa wahajiri wa nchi hizo kuingia Marekani.
Matamshi ya kuchukiza ya Rais Donald Trump yalikabiliwa na radiamali kali kutoka kwa jamii ya walimwengu hususan viongozi wa nchi za Kiafrika, kiasi kwamba kwa mara ya kwanza mabalozi wa nchi 54 za Kiafrika katika Umoja wa Mataifa walitoa taarifa ya pamoja ya kulaani matamshi hayo ya kibaguzi na udhalilishaji ya rais wa Marekani dhidi ya mataifa ya Afrika na Wamarekani wenye asili ya Afrika wanaoishi nchini humo. Katika taarifa hiyo, mabalozi wa nchi za Kiafrika wanaowakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa walimtaka Trump kuomba radhi na kufutilia mbali matamshi yake ya udhalilishaji dhidhi ya mataifa ya bara hilo. Kadhalika viongozi na maseneta wengi wa Marekani nao wametoa radiamali kali kuhusiana na matamshi hayo ya Trump. Kwa mfano Dick Durbin, seneta wa jimbo la Illinois alinukuliwa akisema kuwa, matamshi ya Trump ni ya kibaguzi na yenye kuchukiza mno.
Licha ya kupita zaidi ya wiki mbili tangu rais huyo wa Marekani atoe matamshi hayo ya kibaguzi, bado radiamali zinaendelea kutolewa katika ngazi za kimataifa. Kuhusiana na suala hilo Moussa Faki Mahamat Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema: “Viongozi wa bara la Afrika hawawezi kunyamanzia matamshi machafu na ya udhalilishaji ya rais wa Marekani kuzihusu nchi za Afrika na Haiti.” Mwisho wa kunukuu. Katika uwanja huo si tu kwamba Trump hakualikwa katika mkutano wa 30 wa viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, bali hata wakati anahutubia mkutano wa Davos, viongozi wengi wa Kiafrika waliondoka katika ukumbi wa mkutano huo wakionyesha upinzani na kutoridhishwa kwao na matamshi ya rais huyo wa Marekani. Radiamali za viongozi wa Afrika zinaenedelea katika hali ambayo kwa miongo kadhaa sasa wamekuwa chini ya udhibiti wa siasa na uingiliaji wa moja kwa moja wa Marekani na washirika wake wa Magharibi, suala ambalo limeziletea nchi hizo taathira hasi za migogoro ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi.
Hivi sasa radiamali kali na masisitizo mtawalia ya viongozi wa Afrika yamemlazimu Trump kurejea nyuma, kuomba msamaha na kutangaza kidhahiri kuheshima viongozi wa Afrika na raia wa mataifa hayo, ikiwa ni katika jitihada zake za kufidia uharibifu aliofanya kupitia matamshi yake, kwa kumtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje kwenda Afrika. Licha ya kwamba Rais Donald Trump wa Marekani katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi huko Davos nchini Uswisi alidai kwamba nara yake ya ‘Marekani Kwanza’ haina maana ya kujitenga na dunia, hata hivyo hatua yake ya kuomba radhi kutokana na kutengwa na viongozi wa nchi za Kiafrika hasa baada ya matamshi yake ya udhalilishaji, inaonyesha kwamba siasa za rais huyo, hususan nara yake hiyo ya ‘Marekani Kwanza’, si tu kwamba si sahihi, bali zimeipelekea nchi hiyo kutengwa taratibu na dunia.