Uamuzi wa Afrika wa kurejesha amani kieneo na kimataifa
Wakuu wa nchi za Afrika wamechukua uamuzi wa kuzidisha jitihada kwa ajili ya kurejesha amani katika uga wa kieneo na kimataifa.
Shirika la habari la Anatolia limeripoti kutoka Khartoum kuwa katika uamuzi wao huo, wakuu wa nchi za Afrika wamejadilii masuala kama magendo ya binadamu, madawa ya kulevya, mapambano dhidi ya ugaidi na kuondoa vizuizi vilivyopo katika njia ya amani na usalama wa kieneo na kimataifa. Uamuzi huo umechukuliwa katika kikao pambizoni mwa Mkutano wa 30 wa Wakuu wa Nchi za Afrika huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, viongozi wa nchi za Afrika wamesema kuwa kuna udharura kwa nchi za Afrika kukabiliana na vizuizi kupitia kushirikiana nchi hizo na kuendesha mapambano na changamoto zilizopo.
Tarehe 15 mwezi Januari mwaka Mawaziri wa Fedha wa nchi kumi za Afrika pia wanaoziwakilisha nchi kadhaa za Kiafrika walikutana katika kikao huko Kigali mji mkuu wa Rwanda ambapo walisisitizia ulazima wa kujitegemea nchi za bara hilo.
Washiriki katika mkutano wa Kigali waliitaja hatua ya nchi za Kiafrika ya kuendelea kupokea misaada kutoka nchi za Magharibi kuwa ni kikwazo kwa maendeleo na ustawi wa bara hilo; na kuitaja misaada hiyo kuwa wenzo unaotumiwa na nchi za Magharibi kwa ajili ya kuimarisha ukoloni mamboleo katika nchi za Kiafrika.