Misri yawahukumu maisha jela wanachama wa Ikhwani
(last modified Wed, 31 Jan 2018 03:22:58 GMT )
Jan 31, 2018 03:22 UTC
  • Misri yawahukumu maisha jela wanachama wa Ikhwani

Katika kile kinachoonekana na mwendelezo wa hukumu za kidhalimu dhidi ya wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri, Mahakama ya Jinai ya Cairo imewahukumu kifungo cha maisha jela wanachama sita wa harakati hiyo.

Shirika la habari la nchi hiyo MENA limeripoti kuwa, wanachama hao wa Ikhwanul Muslimin wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya utumiaji mabavu ya mwaka 2015 nchini humo, likiwemo jaribio la kuua maafisa usalama.

Washukiwa wengine wanne wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, huku wengine wawili wakihuumiwa miaka mitano jela katika hukumu zilizosomwa jana Jumanne.

Mapema mwezi huu, Mamlaka ya Magereza ya Misri ilitekeleza hukumu ya kuwanyonga watu watano wakiwemo wanne waliopatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya bomu yalioua maafisa usalama miaka miwili iliyopita, siku chache baada ya kuwanyonga watu wengine 15 waliopatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi yaliyoua askari usalama huko kaskazini mwa Peninsula ya Sinai.

Baadhi ya wanachama wa Ikhwani waliohukumiwa vifungo jela

Tangu alipoondolewa madarakani Muhammad Mursi, rais wa zamani wa Misri aliyechaguliwa na wananchi mwaka 2012, mamia ya wafuasi wa kiongozi huyo wamehukumiwa vifungo tofauti vikiwemo vya maisha jela, huku wengine pia wakihukumiwa adhabu ya kifo na mahakama za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukikosoa hukumu hizo na kusisitiza kuwa, hazijawahi kushuhudiwa katika historia ya sasa. Aidha serikali ya sasa ya Rais Abdel Fattah el-Sisi inatajwa kuwa ya kidikteta na kandamizi dhidi ya wapinzani.

Tags