Marais wanne wa Afrika, wahanga wa vitendo vya wake zao wenyewe
Gazeti moja la Kiarabu limechapisha makala inayoonesha namna marais wanne wa nchi za Afrika walivyokuwa wahanga wa vitendo vya wake zao na baadhi yao hata kupoteza nafasi zao za uongozi.
Katika toleo lake la jana Jumapili, gazeti la al Quds al Arabi limeandika: Mwanamke wa kwanza ni Grace Mugabe, ambaye kwa ghururi na kiburi chake amesababisha ugomvi baina ya mumewe, Robert Mugabe, rais wa zamani wa Zimbabwe na maveterani wenzake na hatimaye kuondolewa kwa nguvu madarakani. Si hayo tu, lakini ubadhirifu mkubwa wa fedha uliokuwa unafanywa hadharani na Grace Mugabe, umemuharibia sana mumewe Robert Mugabe.
Kwa mujibu wa gazeti la al Quds al Arabi, mwanamke wa pili ni Constancia (Mangue) Teodoro Nguema, mke wa Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equtorial Guinea ambaye vitendo vyake viovu vya chini kwa chini na vya siri vinamuharibia sana mumewe.
Mwengine kwa mujibu wa gazeti hilo la Kiarabu ni Simone (Ehivet) Gbagbo, mke wa rais wa zamani wa Kodivaa (Ivory Coast) Laurent Gbagbo ambaye ufisadi wake wa mali ya umma na ubadhirifu ulikuwa maarufu na hatimaye kumfanya mumewe apinduliwe kidhalili na kupelekwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Gazeti hilo la al Quds al Arabi pia limeandika, mwanamke mwingine ni Leïla Trabelsi Ben Ali, mke wa rais wa zamani wa Tunisia Zain el Abidine Ben Ali aliyepinduliwa na wananchi. Moja ya masuala yaliyomchafulia jina sana Ben Ali ni ufisadi na ubadhirifu wa kuchupa mipaka wa mkewe, Leïla Ben Ali.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mbali na wake wa nchi hizo nne, wengi wa wake wa nchi nyingine nao wana sifa hizo hizo na kuna hatari wakawafanya wahanga waume zao.