Indhari ya WFP kuhusu kuenea njaa kusini mwa Afrika
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP) limetahadharisha kuhusu kuenea njaa eneo la kusini mwa Afrika.
Taarifa hiyo ya WFP imesema uhaba wa mvua na wadudu wanaoharibu mimea ya mazao ndiyo sababu itakayolitumbukiza eneo la kusini mwa Afrika katika maafa ya njaa huku mamilioni ya watu wakiwa katika hatari, hasa watoto wadogo.
Eneo hilo kubwa linaloanzia Afrika Kusini hadi Zambia, limekumbwa na joto kali na uhaba wa mvua huku viwavi jeshi vikiharibu mimea na kupunguza mazao ya nafaka katika mwaka 2018.
WFP pia inasema kuna uwezekano wa kuongezeka watu wanaohitajia misaada ya dharura ya chakula ambao idadi yao ilikuwa milioni 26 mwaka jana.
Hayo yanaripotiwa wakati ambao mji wa Cape Town wa Afrika Kusini umezindua kituo cha kukabiliana na maafa DOC ili kujiandaa na hali mbaya kabisa iliyosababishwa na ukosefu wa maji katika mji huo muhimu wa bandari.
Habari zinasema maji ya mabomba yatakatwa kama kina cha maji kwenye mabwawa kitafika ngazi ya asilimia 13.5. Kwa sasa kiwango cha maji kwenye mabwawa kimefikia asilimia 26.7, na kama hali itaendelea kama ilivyo kiwango cha maji kitafikia asilimia 13.5 ifikapo Aprili 12.
Afrika Kusini inapanga kutangaza kiangazia kinachoshuhudiwa maeneo ya magharibi na kati mwa nchi hiyo kuwa maafa ya kitaifa.