Amnesty yakosoa ukandamizaji wa serikali ya Misri dhidi ya wapinzani
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekosoa ukandamizaji unaofanywa na maafisa wa serikali ya Misri dhidi ya wapinzani wa serikali ya nchi hiyo.
Mkurugenzi wa Kampeni za Kimataifa wa Amnesty International kanda ya kaskazini mwa Afrika, Najia Bounaim amesema kuwa, maafisa wa serikali ya Misri wanapaswa kutoa maelezo kamili kuhusu alikopelekwa Naibu Mwenyeliti wa chama cha Misri Yenye Nguvu na kuamuachia huru kama atakuwa ametiwa nguvuni. Najia Bounaim ameongeza kuwa, kutiwa nguvuni mwanasiasa huyo ni hujuma dhidi ya uhuru wa kujieleza.
Katika siku za hivi karibuni maafisa wa serikali ya Misri wamekuwa wakikandamiza viongozi wa vyaka vya upinzani na wanaharakati wa masuala ya kisiasa na uhuru wa kijamii.
Muhammad al Qasaas ni mwanasiasa wa upinzani wa tatu kutiwa nguvuni katika wiki moja ya hivi karibuni nchini Misri.
Wagombea kadhaa wa vyama vya siasa vya upinzani wamejiengua katika kinyang'anyiro cha kugombea kiti cha rais wakilalamikia mashinikizo na ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya dola. Miongoni mwa wanasiasa wa upinzani waliotiwa nguvuni ni Sami Hafez Anan, mkuu wa zamani wa jeshi la Misri aliyekuwa ametangaza kuwa atachuana na Rais Abdel Fattah al al Sisi katika uchaguzi ujao.
Uchaguzi wa rais wa Misri umepangwa kufanyika tarehe 26 hadi 28 za mwezi Machi mwaka huu.