Mashirika ya kutetea haki yautaja uchaguzi ujao wa Misri kama kichekesho
(last modified Wed, 14 Feb 2018 03:21:23 GMT )
Feb 14, 2018 03:21 UTC
  • Mashirika ya kutetea haki yautaja uchaguzi ujao wa Misri kama kichekesho

Mashirika 14 ya kieneo na kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameutaja uchaguzi ujao wa rais nchini Misri kama mchezo wa kuigiza.

Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo yakiwemo Human Rights Watch na Kamisheni ya Kimataifa ya Wanasheria ICJ imekosoa vikali hatua ya vyombo vya dola kukanyaga uhuru na haki za wananchi, sambamba na kuwatia mbaroni au kuwatishia wanasiasa walioonyesha azma ya kugombea urais.

Mashirika hayo yamesema uchaguzi ujao wa Misri haujafikia viwango vinavyohitajika vya kimataifa ili uhesabike kuwa huru na wa haki, huku yakizitaka nchi za Magharibi waitifaki wa Cairo kukosoa uchaguzi huo yanayoutaja kuwa kichekesho. 

Katika siku za hivi karibuni maafisa wa serikali ya Misri wamekuwa wakikandamiza viongozi wa vyama vya upinzani na wanaharakati wa masuala ya kisiasa na uhuru wa kijamii. 

Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri na mwenzake wa Marekani Donald Trump

Wagombea kadhaa wa vyama vya siasa vya upinzani wamejiengua katika kinyang'anyiro cha kugombea kiti cha rais wakilalamikia mashinikizo na ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya dola.

Miongoni mwa wanasiasa wa upinzani waliotiwa nguvuni ni Sami Hafez Anan, mkuu wa zamani wa jeshi la Misri aliyekuwa ametangaza kuwa atachuana na Rais Abdul Fattah al al-Sisi katika uchaguzi ujao wa Misri,  unaotazamiwa kufanyika tarehe 26 hadi 28 za mwezi Machi mwaka huu.   

Tags