Uingereza kuwatimua maelfu ya wahajiri wa Zimbabwe
Serikali ya Uingereza imetangaza azma yake ya kuwafukuza nchini humo maelfu ya wahajiri haramu raia wa Zimbabwe.
Duru za habari zinasema kuwa, Catriona Lang, Balozi wa Uingereza mjini Harare hivi karibuni alimpa taarifa Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Kembo Mohadi kuhusu mpango wa serikali ya London wa kuwatimua wahajiri haramu wapatao 2,500 raia wa Zimbabwe walioko nchini Uingereza kinyume cha sheria.
Tangazo hilo limekuja katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Therea May hivi karibuni alitangaza mpango wa serikali yake wa kuwapunguza 'kwa maelfu' wahajiri wanaoingia nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti ya AFP, kuna takriban Waingereza 20 elfu wanaoshi nchini Zimbabwe, huku raia wa Zimbabwe wanaoshi nchini Uingereza wakikisiwa kuwa zaidi ya laki moja.
Uhusiano wa Zimbabwe na mkoloni wake wa zamani Uingereza haujakuwa wa kuridhisha tangu wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, Robert Mugabe.