UN yasema itaendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya al-Shabaab Somalia
(last modified Sun, 25 Feb 2018 15:29:05 GMT )
Feb 25, 2018 15:29 UTC
  • UN yasema itaendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya al-Shabaab Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sambamba na kulaani mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni yaliyoua makumi ya watu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, amesisitiza kuwa umoja huo utaendelea kuunga mkono jitihada za kulitokomeza kundi la kigaidi na la ukufurishaji la al-Shabaab.

Katika taarifa yake, Antonio Guterres ametoa mkono wa rambirambi kwa familia za wahanga wa hujuma hiyo, na kwa serikali na taifa la Somalia kwa ujumla. Mashambulizi hayo ya Ijumaa iliyopita, yaliua na kujeruhi watu wasiopungua 80.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, UN itaendelea kuiunga mkono na kushirikiana na serikali ya Somalia katika juhudi zake za kuliangamizi genge hilo la wakufurishaji, kwa shabaha ya kuhakikisha amani na utulivu unarejea katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Watu 45 wamethibitishwa kuuawa hadi sasa na wengine 36 kujeruhiwa katika mashambulio hayo ya kigaidi.

Wananchi wa Somalia wakikimbia baada ya kusikia sauti za miripuko mjini Mogadishu siku ya Ijumaa

Mabomu yaliyokuwa yametegwa ndani ya magari mawili yaliripuka sambamba na kujiri shambulizi la ufyatuaji risasi karibu na Ikulu ya Rais Mohammed Abdullahi Mohamed wa nchi hiyo na kusababisha hali ya mtafaruku siku ya Ijumaa. 

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabab limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi ya mjini Mogadishu.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa, vitendo vya kigaidi vya al-Shabaab nchini Somalia vimeua watu zaidi ya elfu mbili na kujeruhi wengine elfu mbili na mia tano, tokeo mwezi Januari 2016 hadi hivi sasa. 

Tags