IGAD yaunga mkono vikwazo dhidi ya wanaovuruga amani Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41053-igad_yaunga_mkono_vikwazo_dhidi_ya_wanaovuruga_amani_sudan_kusini
Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imetangaza kuwa inaunga mkono hatua ya kuwekewa vikwazo viongozi na shakhsia wote wanaokwamisha jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 02, 2018 04:09 UTC
  • IGAD yaunga mkono vikwazo dhidi ya wanaovuruga amani Sudan Kusini

Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imetangaza kuwa inaunga mkono hatua ya kuwekewa vikwazo viongozi na shakhsia wote wanaokwamisha jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro nchini Sudan Kusini.

Hayo yalisemwa jana Alkhamisi kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Mjumbe Maalumu wa IGAD nchini Sudan Kusini, Ismail Wais ambaye ameongeza kuwa, asasi hiyo ya kikanda inaunga mkono hatua zote za kufunga akaunti za benki za wanasiasa na makamanda wa zamani wa kijeshi wanaochochea mapigano katika nchi hiyo changa zaidi duniani. 

Amesema jumuiya hiyo ya kieneo haitaacha kuwachukulia hatua wanaovuruga makubaliano hayo kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa yaliyopitishwa na wakuu wa nchi za IGAD Novemba 24 mwaka 2014.

Amesisitiza kuwa, wanaovunja makubaliano hayo ya amani wanapaswa pia kuwekewa vikwazo vya kusafiri kwenye nchi za kieneo, sambamba na kufungiwa njia zote za kupenyeza silaha zinazoweza kuendelea kuwa chachu ya umwagikaji wa damu nchini humo.

Rais Salva Kiir (kushoto) na Riek Machar

Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, Moussa Faki, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema umoja huo utawawekea vikwazo wale wote wanaokwaza na kutatiza juhudi za kurejesha amani na usalama nchini Sudan Kusini.

Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Vita hivyo vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.