Wananchi wa Ethiopia wafanya mgomo kulalamikia 'hali ya hatari'
Shughuli za kawaida zimelemazwa kutokana na mgomo wa wananchi wa Ethiopia katika mji mkuu Addis Ababa na miji mingine, wanaolalamikia sheria ya hali ya hatari kwa muda wa miezi sita kufuatia kujiuzulu Waziri Mkuu Hailemariam Desalign.
Mgomo huo ulioanza jana Jumatatu umesababisha maduka na vituo vingine vya biashara kufungwa huku barabara zikisalia tupu, hususan katika mji mkuu na miji mingine iliyoko katika eneo la Oromia.
Foleni ya malori ya mizigo na mabasi matupu ya abiria yameonekana katika barabara zinazoingia na kutoka mjini Addis Ababa, huku madereva wakihofia kushabuliwa na wananchi wanaofanya mgomo.
Mgomo huu uliitishwa na asasi ya kiraia iliyopigwa marufuku ya Oromia Media Network, kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Jawar Mohammed ambaye aliendesha kampeni hizo kwenye mitandao ya kijamii hususan Facebook.

Katikati ya mwezi uliopita wa Februari na katika hatua ya kushangaza, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalign alitangaza kujiuzulu wadhifa huo katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni ya taifa, ikiwa ni mara ya kwanza katika zama za sasa kushuhudiwa waziri mkuu aliyeko madarakani nchini humo akichukua uamuzi wa kung'atuka madarakani.
Alisema machafuko na migogoro ya kisiasa imesababisha kupotea maisha na makazi ya watu wengi na kwamba kujiuzulu kwake ni hatua muhimu kwa jitihada za kufanya mageuzi ambayo yataielekeza nchi hiyo kwenye amani endelevu na demokrasia.
Viongozi wa mrengo unaotawala nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wanakutana wiki hii kumteua Waziri Mkuu mpya.