UN yakosoa ukandamizaji Misri kuelekea uchaguzi wa rais
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amekosoa mazingira ya vitisho, ukandamizaji na kuwekewa mbinyo wanasiasa wa upinzani nchini Misri kuelekea uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Katika ripoti ya kila mwaka aliyoikabidhi Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa jana Jumatano, Zeid Ra'ad al-Hussein amesema serikali ya Cairo imejenga mazingira ya kutisha kuelekea uchaguzi huo, kwa kubinya vyombo vya habari, kuwanyanyasa, kuwakamata na kuwazuilia wapinzani.
Amesema ni jambo lisilokubalika namna wagombea wa urais wa vyama vya upinzani walivyoshinikizwa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho, baadhi yao wakikamatwa na kuzuiliwa jela.
Hivi karibuni, Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri alivionya vyombo vya habari vya nchi hiyo dhidi ya kuchafua sura ya vyombo vya usalama.
Hii ni katika hali ambayo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa taarifa likiwakosoa viongozi wa Misri kwa hatua yao ya kuwatia mbaroni kiholela wanasiasa wa upande wa upinzani katika kukaribia uchaguzi wa rais nchini humo.
Uchaguzi wa tatu wa rais wa Misri tangu baada ya kupinduliwa dikteta Hosni Mubarak unatarajiwa kufanyika tarehe 26 na 27 za mwezi huu wa Machi 2018.