Waislamu waandamana Nigeria wakitaka kuachiwa huru Sheikh Zakzaky
Waislamu nchini Nigeria wamefanya maandamano ya amani huko Abuja mji mkuu wa nchi hiyo wakishinikiza kuachiwa huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Ijumaa ya leo wafanya maandamano walimiminika katika mitaa ya mji Abuja wakipiga nara za kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Zakzaky na wafuasi wake kadhaa walioshikiliwa jela. Waandamanaji hao wamelaani jinai alizofanyiwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, familia na wafuasi wake na kusisitiza juu ya ulazima wa kuachiwa huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Sheikh Zakzaky, mkewe na wanachama kadhaa wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walitiwa mbaroni tarehe 13 mwezi Disemba mwaka 2015 kufuatia shambulio lililofanywa na jeshi katika Husseiniya ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria. Mamia ya Waislamu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Ibrahim Zakzaky waliuawa shahidi katika shambulio hilo la jeshi la Nigeria.
Mahakama Kuu ya Nigeria imeagiza kuachiwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe, lakini jeshi la serikali ya nchi hiyo limekataa kutekeleza agizo hilo licha ya maradhi ya kudhoofika kimwili kwa mwanazuoni huyo.