Rwanda yaitaka Burundi ifafanue kuhusu kifo cha mwanadiplomasia wake wa zamani
Rwanda imeitaka serikali ya Burundi kueleza chanzo cha kifo cha balozi wa zamani wa nchi hiyo nchini Ubelgiji na Ufaransa Jacques Bihozagara.
Mwanadiplomasia huyo aliaga dunia Jumatano mchana kwa sababu isiyofahamika katika gereza la Mpimba nchini Burundi, miezi minne baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuifanyia ujasusi nchi yake.
Mazingira ya kifo chake bado hayajulikani, na serikali ya Burundi haijajibu matakwa ya Rwanda.
Bihozagara ambaye aliwahi kuwa waziri wa vijana wa Rwanda na balozi wa nchi yake katika nchi za Ubelgiji na Ufaransa alitiwa nguvuni Desemba 4, 2015 na Shirika la Upelelezi la Taifa la Burundi (National Intelligence Service (SNR)) linalodhibitiwa moja kwa moja na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi. Bihozagara alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kufanya ujasusi kwa maslahi ya shirika la ujasusi la Rwanda.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imetangaza kuwa imeshtushwa na habari ya kifo cha mwanadiplomasia huyo wa zamani na kusisitiza kuwa, serikali ya Burundi inapaswa kutoa majibu kuhusu mazingira na sababu za kifo chake.
Uhusiano wa Rwanda na Burundi ulivurugika baada ya Rais Nkurunziza kuituhumu Rwanda kwamba inawasaidia waasi wanaotaka kuiondoa madarakani serikali yake. Rwanda inakanusha madai hayo.
Hivi karibuni pia, chama tawala nchini Burundi cha CNDD-FDD kimemtuhumu Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwa anataka "kuhamisha" mauaji ya kimbari, huku uhusiano kati ya nchi mbili hizo jirani ukizidi kuharibika.