Wananchi Ghana wapinga mkataba wa kijeshi na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42352-wananchi_ghana_wapinga_mkataba_wa_kijeshi_na_marekani
Maelfu ya watu waliandamana katika mji mkuu wa Ghana, Accra siku ya Jumatano kupinga mkataba tata wa kijeshi baina ya nchi yao na Marekani.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 29, 2018 01:56 UTC
  • Wananchi Ghana wapinga mkataba wa kijeshi na Marekani

Maelfu ya watu waliandamana katika mji mkuu wa Ghana, Accra siku ya Jumatano kupinga mkataba tata wa kijeshi baina ya nchi yao na Marekani.

Mkataba huo ambao ulipitishwa na bunge wiki iliyopita na kisha kuidhinishwa na Rais Nana Akufo-Addo siku ya Ijumaa unakosolewa vikali na wananchi pamoja na vyama vya upinzani kutokana na kuwa unakiuka mamlaka ya kujitawa nchi hiyo.

Serikali za Ghana na Marekani zimefikia mapatano ya kuimarisha uhusiano wa kijeshi huku kukiwa na tetesi kuwa Marekani inapanga kujenga kituo kikubwa cha kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Hata hivyo wakuu wa Accra na Washington wamekanusha kauli hizo.

Rais wa zamani wa Ghana John Mahama wa chama cha upinzani cha NDC amesema anapinga vikali mapatano hayo baina ya serikali ya nchi yake na Marekani.

Maandamano mjini Accra kupinga mkataba wa kijeshi wa Marekani na Ghana

Siku ya Jumanne polisi walimtia mbaroni mwanachama wa ngazi za juu wa NDC , Koku Anyidoho ambaye alisema mkataba huo utapelekea kuibuke mapinduzi ya wananchi.

Katika miezi ya hivi karibuni Marekani imekuwa ikijaribu kuimarisha satwa yake ya kijeshi katika nchi kadhaa za Kiafrika kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.