UN: Ni hatari kufanyika uchaguzi sasa hivi nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42476-un_ni_hatari_kufanyika_uchaguzi_sasa_hivi_nchini_libya
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa, ni hatari kufanyika uchaguzi katika mazingira ya hivi sasa nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2018 23:39 UTC
  • UN: Ni hatari kufanyika uchaguzi sasa hivi nchini Libya

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa, ni hatari kufanyika uchaguzi katika mazingira ya hivi sasa nchini Libya.

Ghassan Salamé amesema hayo na kuongeza kuwa, licha ya kwamba ni jambo la dharura kuhakikisha uchaguzi unafanyika nchini Libya kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2018 lakini pamoja na hayo kuna hatari uchaguzi huo ukazidisha matatizo ya kiusalama ya Libya badala ya kuyatatua.

Amesema, kufanyika uchaguzi wa rais nchini Libya bila ya kuweko Katiba inayokubaliwa na wote, ni jambo gumu sana.

Hali bado si shwari nchini Libya

 

Vile vile amesisitiza kuwa, juhudi zozote za kuyaunganisha makundi ya kisiasa na kurejesha umoja na mshikamano nchini Libya hazitofanikiwa maadamu wizi wa mali ya uma na uhalifu mwingine kama utakatishaji fedha, magendo ubadhirifu n.k, umeshika kasi nchini humo.

Matamshi ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya yametolewa katika hali ambayo tarehe 21 Machi alisema kuwa Umoja wa Mataifa unalipa kipaumbele suala la kufanyika uchaguzi wa kiuadilifu, huru na salama kabla ya kumalizika mwaka huu nchini Libya.

Uchaguzi wa bunge ndio uliokuwa wa mwisho kufanyika nchini Libya mwaka 2014 na matokeo ya uchaguzi huo ni kuzuka mzozo mkubwa uliopelekea nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kuwa na mabunge mawili na serikali mbili tofauti.