Al Shabab yashambulia kambi ya Umoja wa Afrika karibu na Mogadishu
Wanamgambo wa kundi la al Shabab leo wamepigana kwa masaa kadhaa na wanajeshi wa Umoja wa Afrika baada ya kulipua gari walilotega bomu ndani yake nje ya kambi ya wanajeshi hao.
Wanamgambo hao mapema leo waliishambulia kambi ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Bula Marer umbali wa kilomita 130 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Hayo yameelezwa na wakazi wa mji huo. Tangu lilipofurushwa huko Mogadishu mwaka 2011, kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida limepoteza udhibiti wa miji na vitongoji vingi nchini Somalia.
Farah Osman Meja katika jeshi la Somalia aliyeko karibu na kambi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM) nchini Somalia ameripoti kuwa wanamgambo wa al Shabaab kwanza walilipua mabomu mawili waliyokuwa wametega garini ambapo moja limeidhuru gari ya AU na jingine lililenga gari la jeshi la Somalia. Ameongeza kuwa baada ya hapo idadi kubwa ya wanamgambo wa kundi hilo walianza kufyatua risasi kutokea katika miti. Meja Osman amesema vilikuwa vita hatari mno.
Wakati huo huo Kanali Muhyiddin Yasin kutoka jeshi la Somalia amesema kuwa mapigano yalizuka leo asubuhi wakati wanamgambo wa al Shabab walipofanya shambulio la kuvizia dhidi ya kikosi cha AMISOM katika wilaya ya Bula Marer inayopatikana katika mkoa wa Shabelle ya chini. Amesema kuwa wanamgambo wa al Shabaab waliuvamia msafara wao wa wanajeshi huko Bula Marer.
Ali Nur Naibu Gavana wa mkoa wa Shabelle ya chini kwa upande wake amesema kuwa wanajeshi 23 wa kikosi cha AMISOM wameuawa pamoja na mwanajeshi mmoja wa jeshi la Somalia katika mapigano hayo.